SALAMU ZA MWAKA MPYA 2026 KUTOKA KWA MWENYEKITI WA TANZANIA BLOGGERS NETWORK (TBN)

Wednesday, December 31, 2025
TBN

 

Ndugu Wasomaji na Watumiaji wa Blogu Tanzania.

Tunapouaga mwaka 2025, nachukua fursa hii, kwa niaba ya wanachama wote wa Tanzania Bloggers Network (TBN), kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa kumaliza mwaka huu "kibabe". 

Tumekuwa na mwaka wenye matukio mengi ya kihistoria, na ninyi wasomaji wetu mmekuwa wadau muhimu kwa kufuatilia habari, uchambuzi, na taarifa mbalimbali kupitia majukwaa yetu ya kidijitali.

Kuelekea Mwaka 2026: Makubwa Zaidi Yanakuja! Mwaka 2026 unakwenda kuwa mwaka wa mageuzi makubwa kwa TBN. Tunatarajia kuleta maudhui yenye ubunifu wa hali ya juu, habari za kina, na teknolojia ya kisasa zaidi katika kuhabarisha umma. Wanachama wetu wamejipanga kuwa daraja imara zaidi kati ya serikali na wananchi, tukihakikisha kila Mtanzania anapata habari sahihi na kwa wakati.

Ombi Langu kwa Watanzania: Tunapoingia 2026, rai yangu ni kuendelea kudumisha amani na utulivu. Tuepuke vurugu na migawanyiko, badala yake tujikite katika umoja wetu kama Taifa. Huu ni wakati wa kuungana kwa nguvu moja kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Vision 2050). Lengo letu ni moja: kuhakikisha kila Mtanzania, kuanzia mjini hadi vijijini, anafaidi "keki ya taifa" na kupata maendeleo ya kweli.

Mwaka 2026 uwe mwaka wa neema, baraka, na mafanikio tele katika kazi na shughuli zenu za kila siku.

Heri ya Mwaka Mpya 2026! 

Beda Msimbe 

Mwenyekiti, Tanzania Bloggers Network (TBN).

MSIGWA AIPONGEZA TCRA KWA KUWALEA TBN NA WAANDISHI WA MITANDAONI

Thursday, December 18, 2025


Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kulea na kuwawezesha waandishi wa habari wa mitandaoni na mabloga, badala ya kuwashughulikia kwa mtazamo wa adhabu, ili kujenga tasnia imara na yenye tija ya habari nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwelekeo wake wa kulea wadau wa sekta ya habari badala ya kuchukua hatua kali za kinidhamu.

Msigwa alisema mwelekeo huo unaendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali kwa manufaa ya taifa.

Aliitaja Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuwa ni wadau wakubwa wa serikali katika tasnia ya habari, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kusambaza taarifa na kujenga mawasiliano kati ya serikali na wananchi.

“Serikali imewaamini waandishi wa mitandaoni, sasa nanyi muendelee kuonesha imani kwa serikali. Ushirikiano wetu umeendelea kuimarika na changamoto zinazojitokeza tunazitatua kwa pamoja,” alisema Msigwa.

Akikanusha madai kuwa waandishi wa habari wa mitandaoni ni dhaifu, Msigwa alisema wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na wana nafasi kubwa ya kutumia kalamu zao kujenga taifa.

“Nimekuwa nikisisitiza waandishi tutumie kalamu zetu kujenga nchi. Mnafanya kazi sahihi na mnalinda maslahi ya taifa,” aliongeza.

Msigwa aliwahakikishia waandishi ulinzi wa serikali, akisema endapo sheria, kanuni au sera zitabainika kuwa kikwazo katika utendaji wao, zitafanyiwa marekebisho kwa maslahi mapana ya taifa.

Alitangaza pia kuanza kwa maandalizi ya mafunzo kwa waandishi wa habari kwa kushirikiana na TCRA, akiwataka kuyapokea kwa mtazamo chanya kama sehemu ya kuongeza weledi na taaluma.

Kuhusu masuala ya kodi, Msigwa alisema serikali itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa mitandaoni, akitambua mchango wao katika kuitangaza nchi na kuvutia uwekezaji.

Aidha, alieleza kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ipo katika mchakato wa kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwawezesha waandishi wa habari, hususan wa mitandaoni.

Akizungumzia mazingira ya sasa ya kimataifa, Msigwa alisema vita vya dunia ya sasa vimehama kutoka silaha za kijeshi kwenda kwenye taarifa, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kulinda na kuipromote nchi.

Aliwahimiza waandishi kuhakikisha majukwaa yao yanatumika kulinda maslahi ya taifa na kuonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao yanayoweza kuharibu taswira ya Tanzania.

Hata hivyo, Msigwa alionesha kusikitishwa na tabia ya baadhi ya waandishi kunyamaza wanapodhalilishwa, akiwataka kusimama na kulinda hadhi ya taaluma yao.








Miaka 64 ya Uhuru: TBN Yasema “Amani Kwanza, Ujenzi wa Taifa Daima”

Tuesday, December 09, 2025

 



Leo Desemba 9, tunapoadhimisha miaka 64 tangu Taifa letu lipate Uhuru, Tanzania Bloggers Network (TBN) inawapongeza Watanzania wote kwa kufikia hatua hii muhimu katika historia ya Taifa letu. Hii ni siku ya kutafakari safari tuliyotoka, mahali tulipo, na mwelekeo tunaoujenga kwa pamoja.


Waasisi wetu walituwachia zawadi kubwa—Uhuru. Lakini walituonya kuwa Uhuru hauwezi kuwa kamili bila kujitegemea. Leo tunakumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza:


"Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi."

 

Tujenge Taifa Letu – Tusiibomoe Tanzania


Kama mtandao wa habari za kidijitali, TBN inasisitiza kuwa mafanikio yetu kama Taifa yametokana na utulivu, umoja na mshikamano. Ili kuendelea mbele, tunahitaji kudumisha amani na maridhiano—nguzo muhimu za maendeleo.

Rais mstaafu Benjamin William Mkapa alituasa kwa busara:


"Amani si kitu cha asili; tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo ya kweli."


Tukikubali kuongozwa na chuki, uchochezi na vurugu, juhudi za waasisi wetu za kupambana na ujinga, umaskini na maradhi zitapotea. Tusiitumie mitandao au uhuru wa maoni kuharibu Taifa letu; tuitumie kulijenga.

Kila Zama na Kiongozi Wake – Tuunge Mkono Mageuzi


Kila kizazi kina wajibu wake. Kama alivyoeleza Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi:


"Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa hili."


Katika awamu ya sasa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea na mwelekeo wa 4R: Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding. Huu ni mwaliko kwa Watanzania wote kushiriki katika kujenga Taifa lenye maridhiano, mageuzi chanya na uimara wa kiuchumi na kijamii.


Tuna nafasi ya kuzungumza—basi tuseme kwa njia inayojenga, si inayobomoa. Kuthamini Uhuru ni kufanya kazi kwa bidii, kulinda amani, na kuacha kutumiwa kuharibu misingi ya Taifa letu.

 

TBN Inawatakia Maadhimisho Mema ya Miaka 64 ya Uhuru!


Tanzania Kwanza — Kazi, Utu na Mshikamano. Tusonge Mbele!


Beda Msimbe

Mwenyekiti, Tanzania Bloggers Network (TBN)

 
Designed By TBN | Developed By Gadiola Emanuel