TBN Yaishukuru Serikali kwa Uamuzi wa kutoa Mafunzo ili Kuimarisha Weledi wao

Friday, July 18, 2025

WhatsApp%20Image%202025-07-09%20at%2021.40.35


Na Mwandish wetu, Dar es Salaam.

CHAMA cha Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) kimeshukuru uamuzi wa serikali ya kuwapatia mafunzo maalumu ya kunoa weledi na uzalendo wa wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Mabloga zaidi ya 200 wakiwemo wa diaspora walioanzisha Mtandao huo mwaka 2015 watapata mafunzo hayo. 


“Tumekuwa na mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao kimsingi ndio wasimamizi wakuu wa maudhui na wametuthibitishia kwamba wapo hatua za mwisho za kutekeleza maagizo ya serikali ya kutoa mafunzo kwa mabloga wote nchini,” alisema Mwenyekiti wa TBN , Beda Msimbe. 


Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Msimbe alisema kwamba lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea mabloga weledi, uzalendo, na umakini katika kutambua na kupambana na habari feki, huku wakiwezesha usambazaji wa taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu ujao. 


“ Tunahitaji kukumbushana kuhusu nchi hii, katiba yetu, amani na umuhimu wa uchaguzi katika demokrasia ya aina yetu.Uamuzi huu wa serikali wa kutupiga msasa ni muhimu sana” alifafanua.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mwenyekiti huyo wa TBN, Beda Msimbe, alieleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali kufanikisha mafunzo. Alisema wameomba mafunzo hayo kipindi cha sasa kwa kuwa wapo wanablogu ambao ni mara ya kwanza kuelekea katika uchaguzi mkuu, na kurejea ombi lao tena wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo. 


Alisema kwamba uongozi wa TBN kwa sasa unafanya kazi kwa karibu na serikali kuhakikisha kuwa zaidi ya wanachama 150 wa chama hicho waliotawanyika nchini kote wanafaidika kikamilifu na mafunzo haya muhimu. 


Msimbe aliwataka mabloga wote nchini kuhakikisha wanawasiliana na Mratibu wa TBN, Bw. Gadiola Emanuel ili kuthibitisha anwani zao na kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kwa ajili ya ushiriki. Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wale wote ambao bado hawajajiunga na TBN kufanya hivyo sasa ili waweze kunufaika na fursa hii muhimu ya mafunzo. 


Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kinajumuisha mabloga wanaotengeneza aina mbalimbali za maudhui, ikiwemo michezo, habari za siasa, afya, uchumi, na habari mchanganyiko. Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha uwezo wao wa kutoa taarifa zenye ukweli na uhakika, hivyo kuchangia katika mazingira ya uchaguzi yenye uwazi na uwajibikaji. 

Serikali Yakubali Kutoa Mafunzo kwa Mabloga Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Friday, July 18, 2025


Gerson

Na Mwandishi Wetu
Serikali imekubali kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa blogu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, hatua muhimu itakayowajengea uwezo na kuwaandaa kubeba dhamana kubwa ya usambazaji wa habari sahihi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa katika Mkutamo wa Wadau Kujadili Mchango wa Sekta ya habari Katika kufanikisha uchaguzi Mkuu 2025.

Katika mkutano huo kipindi cha majadiliano Mwenyekiti wa Chama cha Mabloga Tanzania (TBN), Beda Msimbe, aliomba serikali kuona umuhimu wa kufunza mabloga wengi ambao sio waandishi lakini wanatengeneza maudhui kuwa na weledi kuandika masuala ya siasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam, Julai 9, 2025, Bwana Msimbe alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo mabloga, akibainisha kuwa, "Wao wanabeba dhamana kubwa kutokana na wingi wao na wanatengeneza maudhui, na wengine si waandishi wa habari."

Aliongeza kuwa katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia na akili bandia (AI), vyanzo vya habari vinavyotegemewa zaidi si mitandao ya kijamii, bali maandishi yanayopatikana kwenye blogu na tovuti, hivyo kufanya uhitaji wa mafunzo kuwa mkubwa zaidi.
Bwana Msimbe alitumia fursa hiyo kupongeza uamuzi wa kuandaa kikao hicho muhimu cha wadau, akisema kuwa ni hatua inayostahili kuelekea uchaguzi wa haki na uwazi. Licha ya changamoto ya mada nyingi (tisa) kujadiliwa ndani ya siku moja, alipongeza mkutano huo na jinsi ulivyokwenda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Ndugu Msigwa, aliliagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuandaa mafunzo hayo mapema iwezekanavyo.
Kauli hiyo ya serikali imetafsiriwa na wadau mbalimbali kama hatua ya kutambuliwa rasmi kwa mchango wa mabloga katika tasnia ya habari na katika mchakato wa kidemokrasia.

Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kina wanachama zaidi ya 200 waliotawanyika kote nchini na nchi za nje, hivyo mafunzo haya yatakuwa na athari kubwa katika kuhakikisha usambazaji wa habari sahihi, zenye vigezo vya kitaaluma, na zinazozingatia maadili ya uandishi wa habari wakati wa kipindi cha uchaguzi na baadae.

Mkutano huo ulifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ambaye alitaka vyombo vya habari na vya usalama kuhakikisha Amani na kuvumiliana kuelekea katika uchaguzi huo.
 
Designed By TBN | Developed By Gadiola Emanuel